Wednesday, May 28, 2014

INJINIA ANUSURIKA KUPATA KIPIGO KUTOKA KWA WANANCHI


INJINIA wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Hamis Chande, amenusurika kupigwa na wananchi wa Kijiji cha Bugulula, wilayani Geita baada ya kwenda kuangalia msingi wa jengo la Mama na Mtoto linalodaiwa kujengwa chini ya kiwango.

Tukio hilo limetokea, wakati injinia huyo alipofika kijijini hapo akiwa na mafundi na vifaa  kama saruji na nondo kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa msingi huo ambao ni mbovu, huku wananchi wakitaka ubomolewe wote na uanze upya bila kujali fedha za kurudia watazipata wapi.

Wananchi walipomuona injinia huyo walikwenda eneo hilo, walipiga yowe wakitaka wananchi wakusanyike wapewe majibu ya kutosha kuhusu hatma ya msingi huo, lakini injinia huyo alikosa majibu, hali iliyosababisha wananchi waanze kumzonga wakitaka kumpiga wakidai naye ni wale wanaokula fedha za wananchi kwa kujinufaisha wao wenyewe.

Wakizumgumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema wao hawataki kurekebishwa kwa msingi, bali wanataka ubomolewe na urudiwe kujengwa upya kwani sh milioni 36 ni pesa nyingi  ambazo  wanadai zimejenga msingi huo.

Wakati vurugu hizo zikiendelea, walifika polisi kutoka Kituo Kikuu cha Wilaya ya Geita wakiwa katika gari PT 1166 na kumuamuru injinia kuondoka eneo hilo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ali Kidwaka, alipoulizwa kwanini amemtuma injinia wake kwenda na mafundi wakati aliyetakiwa kwenda ni mkandarasi, alikana kumtuma injinia huyo na mafundi wala  kuzungumza chochote, bali alimtuma akakague na kurudisha majibu.

“Nashaanga kusikia kaenda na mafundi, lakini mimi kama mkurugenzi nasema msingi huo utabomolewa na kujengwa upya,” alisema.

No comments:

Post a Comment