Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani linamshikilia dereva Frank Chabayanga (39) mkazi wa Morogoro wa basi la kampuni ya BM kwa tuhuma za kumgonga mtembea kwa miguu na kusababisha kifo chake.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani Pwani Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Ulrich Matei (pichani) amesema kuwa tukio hilo limetokea Mei 20 mwaka huu majira ya saa 3:30 Usiku eneo la Kwa Mbonde wilayani Kibaha katika barabara kuu ya Dar es Salaam Morogoro.
Kamanda Matei amesema kuwa mtuhumiwa alikuwa akiendesha gari aina ya Yu Tong lenye namba za usajili T 919 CAB alimgonga mtu ambaye jina lake halikuweza kutambuliwa mara moja.
Aidha alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo wa kasi ambapo mwili wa marehemu umehifadhiwa kwnye hospitali ya Rufaa ya Tumbi.
Kwenye tukio lingine dereva Issa Kidito (64) mkazi wa Dar es salaam anashikiliwa kwa tuhuma za kumgonga mpanda baiskeli na kusababisha kifo.
Kamanda Matei amesema kuwa mtuhumiwa alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Land Cruiser hard top lenye namba za usajili namba T 722 ABA aliwagonga wapanda baiskeli na kusababisha kifo cha Mwalimu Hamisi Mtanga (58).
Amebainisha kuwa tukio hilo lilitokea kitongoji cha Londondo Kijiji cha Kiwanga Kata ya Chumbi tarafa ya Muhoro wilaya ya Rufiji ambapo mtuhumiwa huyo alikuwa akielekea mkoani Lindi aliacha barabara na kumgonga mwendesha baiskeli huyo ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi Mihilu na kufariki papo hapo huku abiria wake Mussa Ndolela akijeruhiwa na kulazwa kituo cha afya Muhoro.
No comments:
Post a Comment