Tuesday, May 27, 2014

Larijani abainisha chanzo cha matatizo ya ulimwengu

 

Larijani abainisha chanzo cha matatizo ya ulimwengu
Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu wa Iran yaani bunge amesema kuwa, matatizo mengi yanayojiri ulimwenguni, yanasababishwa na kutozingatiwa masuala ya akili na dini. Akizungumza kwenye sherehe za kufungwa tamasha la kwanza la 'Tuzo Kuu ya Mtume Mtukufu SAW' mjini Tehran, Dakta Ali Larijani amesema kuwa, upotofu mwingi unaoonekana katika ulimwengu wa leo unasababishwa na kutozingatiwa mambo mawili ambayo ni akili na dini, kwani mambo hayo yanakamilishana; na kwamba matatizo hujitokeza pindi linapokosekana moja kati ya mambo hayo. Dakta Larijani ameongeza kuwa, kuna nukta kadhaa muhimu za kuzingatiwa katika suala la kubaathiwa Mtume Mtukufu SAW, ambapo nukta ya kwanza ni tawhidi na kumpewekesha Mwenyezi Mungu SW, na nukta ya pili ni kupambana na ujinga, kwani matatizo mengi ya mwanadamu yanasababishwa na ujinga. Dakta Larijani amesema kuwa, ufisadi kamwe hauwezi kutokomezwa bila ya kuwepo umaanawi na tawhidi; kwani Mtume Mtukufu SAW alianza harakati zake za kuutangaza Uislamu kwa neno la kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Inafaa kuashiria hapa kuwa, tarehe 27 Rajab inasadifiana na siku aliyobaathiwa na kupewa utume, Mtume Muhammad SAW.

No comments:

Post a Comment