Wawakilishi wa waasi wa zamani wa Seleka katika Jamhuri ya Afrika ya Kati hapo jana walikutana na wawakilishi wa jeshi la taifa pamoja na jeshi la Ufaransa katika mji wa Bambari ulioko katikati mwa nchi hiyo. Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kujadili namna ya kukusanywa silaha zilizotapakaa katika nchi hiyo; silaha ambazo zinatumika na makundi mbalimbali kuvuruga amani na utulivu nchini. Msemaji wa Seleka, Kanali Djouma Narkoyo, amesema mazungumzo ya hapo jana yalikuwa mazuri na malengo yake yanaweza kufikiwa iwapo pande zote husika zitaonyesha irada thabiti ya kuyafanyia kazi. Narkoyo ameelezea uungaji mkono wa kundi lake katika suala la kukabidhi na kudhibiti silaha ingawa msemaji huyo wa Seleka ameelezea wasiwasi wake kuhusiana na kundi la waasi wa Kikristo la Anti-Balaka ambalo amesema linahujumu mipango yote ya kukusanywa silaha. Amesema pindi wapiganaji wa Seleka wanapoamua kukabidhi silaha zao, waasi wa Anti-Balaka huanzisha mashambulizi dhidi yao au dhidi ya Waislamu na hivyo inakuwa vigumu kukabidhi silaha katika mazingira kama hayo.
Inafaa kukumbusha hapa kuwa, mwezi Disemba mwaka uliopita, wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka walianzisha vita vya kidini Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo lengo lao kuu lilikuwa ni kuwaua kwa umati Waislamu walio wachache nchini humo. Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali ni kwamba, tangu kuanza vita vya ndani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati hadi sasa, zaidi ya watu milioni moja, wengi wao wakiwa ni Waislamu wameikimbia nchi bila kutaja maelfu ya wengine ambao wameuawa. Takwimu za umoja wa Mataifa zinasema ni watu 2000 ndio waliouawa kwenye machafuko huko CAR ingawa mashirika ya kiraia yanasema idadi ya waliopoteza maisha inapindukia 4000.
Juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanywa kwa lengo la kukomesha mapigano Jamhuri ya Afrika ya Kati lakini hadi sasa hali bado si shwari katika nchi hiyo. Viongozi wa Kiislamu na wale wa Kikristo wamekuwa wakijaribu kuhamasisha wafuasi wao kuwa na subira na uvumilivu na kukaa na wenzao wa upande wa pili kwa amani lakini miito kama hiyo haijaitikiwa na wengi hususan kwa upande wa Wakristo wakiongozwa na wapiganaji wa Anti-Balaka. Hii ni katika hali ambayo, Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika limeonya makundi yenye silaha huko Jamhuri ya Afrika ya Kati kwamba yatakabiliwa na vikwazo iwapo hayatokubali kuweka chini silaha zao. Katika taarifa yake baraza hilo limetahadharisha kuwa, kuendelea hali ya mchafukoge katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kunatishia usalama wa eneo la Maziwa Makuu na bara zima la Afrika kwa ujumla.
Wachambuzi wengi wanasema mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ungekuwa umemalizika kitambo lakini uungaji mkono wa majeshi ya Ufaransa kwa kundi la Kikristo la Anti-Balaka umepelekea kundi hilo kuvimba kichwa na kuendeleza mauaji dhidi ya Waislamu. Baadhi ya taarifa zinaonyesha kuwa wanajeshi wa Ufaransa wamekuwa wakipuuza miito ya Waislamu punde wanapokabiliwa na hatari ya kuuawa na Anti-Balaka na hata wakati mwingine wanashambuliwa na wanajeshi hao wa Ufaransa wanapojaribu kupambana na wanamgambo hao wa Kikristo.
Weledi wa mambo wanasema Jamhuri ya Afrika ya Kati ni nchi muhimu sana kijografia na kistratejia na kwa mantiki hiyo dunia haifai kukaa kimya na kuwa mtazamaji wa mgogoro unaoendelea. Wapembuzi wengi wanataka hatua za dharura zichukuliwe kukomesha kabisa ghasia na machafuko katika nchi hiyo ili kuandaa mazingira ya kurejea amani na utulivu wa kudumu.
No comments:
Post a Comment