Wednesday, May 28, 2014

SHEHE MKUU WA MKOA WA DAR AHAMASISHA WAUMINI KUCHANGIA DAMU


Na Peter Mwenda

WATANZANIA wametakiwa kujitokeza kuchangia damu kwa hiari bila kujali dini zao ili kuokoa maisha ya wajawazito na watoto.

Hayo yalisemwa na Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Shekhe Alhad Salum wakati akizingumza katika semina ya viongozi wa madhehebu ya dini na taasisi zinavyoweza kuhamasisha waumini wao kuchangiaji damu.

"Unapochangia damu unamsaidia mwanadamu mwenzio, hili halina dini wala imani ni watu wachache wanaojitolea kutoa damu kulingana na mahitaji ya wajawazito,watoto na wengine wanaohitaji kuongezewa damu" alisema Shekhe Alhad.

Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili na Tiba Mbadala Tanzania kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Paulo Muhane alisema bado kuna changamoto kubwa ya uchangiaji wa damu kwa sababu kutoka serikali ianzishe mpango wa Damu Salama haijawahi kuvuka lengo la kukusanya chupa 400,000 kwa mwaka.

Alisema mpaka sasa Mpango wa Damu Salama unakusanya chupa 160,000 kwa mwaka na wengi wao wanachangia damu wanapokuwa na wagonjwa hospitalini hivyo aliwaomba viongozi wa kiroho kuwaelimisha waumini wao kuchangia damu kwa hiari.

Dkt.Muhame alisema uchangiaji damu kwa wingi kunakidhi mahitaji kwa vile unaokoa maisha ya wengi ambao wanakufa kwa kukosa damu.

Naye Askofu Dkt. Frederick Kigadye kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) aliwataka baadhi ya watumishi wa umma wanaouza damu hospitalini waache tabia hiyo kwani wanawakatisha tamaa wanaochangia.

"Damu ni uhai, binadamu tunaishi kutumia damu, ili watoto wakue tumboni wanahitaji damu,wajawazito wengi wanatoka damu nyingi wanapojifungua hivyo tuchangie damu kuokoa maisha yao"alisema Dkt. Kigadye. 

Mpango wa Damu Salama uliwaalika viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini,wakuu wa shule na taasisi binafsi  kujadiliana namna ya kuwaelimisha waumini wao kuchangia damu kwa hiari kuokoa jamii inayohitaji kuongezewa damu hospitalini.

No comments:

Post a Comment