Wednesday, May 28, 2014

Malawi;Matokeo ya uchaguzi ni Ijumaa


Tume ya uchaguzi ya Malawi imesema itatangaza matokeo ya uchaguzi ijumaa.
Hatimaye tume ya uchaguzi nchini Malawi imesema itatangaza matokeo ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo kesho ijumaa.
Uamuzi huo unakuja baada ya mivutano na mapingamizi kadhaa kwenye mahakama kuu nchini humo.
Mwandishi wa BBC Baruan Muhuza ameeleza kutoka mji mkuu wa nchi hiyo Lilongwe kuwa sasa wananchi wa Malawi wameondolewa hofu ya kusubiri kwa muda mrefu matokeo ya kura za uchaguzi walioufanya juma lililopita.
Taarifa fupi iliyotolewa na tume ya uchaguzi jana usiku mjini Blantyre, imesema wameamua kutangaza matokeo hayo kwa kuzingatia sheria inayoibana kufanya hivyo ndani ya siku zisizozidi nane na ikiwa ni baada ya saa 48 tangu kumaliza hesabu ya kura.
Kwa siku mbili sasa kumekuwa na tuhuma za kuokotwa kwa baadhi ya masanduku ya kura, huku baadhi ya magari ya yakipatikana na masanduku ya kura na hata katika baadhi ya maeneo ambako ilielezwa kuwa kura zimehifadhiwa, usalama wake umesemwa kuwa mdogo.
Tume ya uchaguzi ya Malawi imesema itatangaza matokeo ya uchaguzi ijumaa.
Tangu jumatatu tume hiyo imekuwa ikisubiri uamuzi wa mahakama kuu mjini Blantyre wa kuiongeza muda wa angalau siku 30 kukamilisha jukumu ililopewa, hata hivyo mahakama yenyewe bado ina mashauri mengine iliyopokea kuhusu uchaguzi huu
Mmoja kati ya wananchi wa nchi hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Malani Nyirenda, alielezea hisia zake alipozungumza na BBC mjini Lilongwe kutokana na suala la kuchelewa kutolewa matokeo na mpango wa kuhesabu upya kura za baadhi ya maeneo.
Tume hiyo imesema hadi kufikia sasa imepokea malalamiko 275 na imekwisha yafanyia kazi malalamiko 170 tu.

No comments:

Post a Comment