Kamisheni maalumu ya mawasiliano inayoshughulikia mambo ya usalama mjini Khartoum, Sudan, imeamuru kupelekwa katika maeneo ya kusini mwa mjini huo wakimbizi wa Sudan Kusini walioelekea nchini humo ili kuokoa maisha yao. Hayo yamebainishwa na kamanda wa jeshi la usalama nchini Sudan Omar Nemr na kuongeza kuwa, uamuzi huo umechukuliwa kufuatia kuwepo malalamiko ya wakazi wanaoishi karibu na kambi hizo za wakimbizi juu ya kuwepo vitendo hasi na tishio la usalama kutoka kwa wakimbizi hao. Ameongeza kuwa, tayari serikali ya Sudan imekwishaandaa mahala maalumu kwa ajili ya kuwekwa mamia ya wakimbizi hao ambao wanaongezeka kila uchao kutokana na kuendelea mapigano kati ya wafuasi wa Rais Salva Kiir Mayardit wa Sudan Kusini na wale wa hasimu wake, Rieck Machar. Kwa upande mwingine Nemr amewataka wakimbizi hao kujiepusha na vitendo vya uhalifu hata kama ni baina yao, katika kipindi watakachokuwa ugenini nchini Sudan. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, zaidi ya raia wa Sudan Kusini elfu 80 walikimbilia nchini Sudan kutokana na mapigano nchini mwao.
No comments:
Post a Comment