Tuesday, May 27, 2014

Safari ya Papa katika eneo na mazungumzo yake na viongozi wa Israel

 

Safari ya Papa katika eneo na mazungumzo yake na viongozi wa Israel
"Israel ni utawala kichaa ambao unapasa uwe chini ya himaya ya kimataifa, kwa sababu kinyume na hivyo utaiangamiza dunia". Hayo ni maneno yaliyosemwa na Askofu Manuel Musallam, mjumbe wa kamati ya Kiislamu na Kikristo ya kusaidia matukufu ya Palestina sambamba na safari ya Papa katika eneo na akaongeza kusema kwamba njama za utawala wa Kizayuni dhidi ya msikiti wa al Aqsa na Kanisa la Qayamat ni utangulizi wa vita vya kidini. Papa Francis, kiongozi wa Wakatoliki duniani ameendelea na safari yake katika eneo la Mashariki ya Kati na kuwasili katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu iliyopewa jina la Israel katika hali ambayo, Wakristo wa eneo hilo kama walivyo wenzao Waislamu wamedhihirisha mbele ya kiongozi wao huyo malalamiko yao dhidi ya siasa za kinyama za Israeli licha ya ulinzi na udhibiti mkali uliofanywa na utawala huo haramu wakati wa safari ya kiongozi huyo wa Wakatoliki. Kabla ya kuelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa ajili ya safari hiyo ya siku tatu, Papa Francis alikuwa nchini Jordan ambako alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo. Shimon Peres, Rais wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo ghasibu ndio waliomlaki kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki. Akizungumza bila ya aibu, Peres alidai katika mazungumzo yake na Papa kwamba Israel ni nchi ya kidemokrasia na ya Kiyahudi, na kwamba watu wenye asili tofauti wanaishi ndani yake kwa amani na masikilizano. Rais wa utawala wa Kizayuni aliielezea Israel kuwa ni mpenda amani na kwamba inafuatilia suala hilo hadi nje ya mipaka yake. Naye Waziri Mkuu wa utawala huo ghasibu Benjamin Netanyahu alisema katika mazungumzo na kiongozi wa Wakatoliki duniani kwamba Papa ameelekea kwenye kitovu cha Mashariki ya Kati chenye misukosuko na machafuko makubwa na kwamba aghalabu ya Wakristo walioko katika hilo wanaudhiwa na kunyanyaswa. Lakini Israel, kwa mujibu wa madai ya Netanyahu, ni kisiwa cha uvumilivu ambacho kinaheshimu haki za dini zote na kwamba eti utawala huo umehakikisha kuwepo uhuru wa kuabudu kwa watu wote; na wenyewe umechukua dhamana pia ya kulinda ufanyaji ibada za kidini katika maeneo matakatifu ya Wakristo, Waislamu na Wayahudi.
Maneno hayo ya uwongo na uzandiki mtupu ya viongozi wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika mazungumzo yao na Papa Francis yametamkwa katika hali ambayo kwa miongo kadhaa sasa ulimwengu unashuhudia unyama na dhulma za waziwazi zinazofanywa na utawala huo haramu katika eneo hili la Mshariki ya Kati. Mauaji, ubomoaji nyumba, uhamishaji watu, ubaguzi, ujenzi wa vitongoji na uvunjiaji heshima matukufu ya Baitul Muqaddas na Palestina kwa ujumla ndivyo vielelezo vinavyotumiwa na walimwengu kuutambulisha utawala haramu wa Israel. Miaka 66 ya kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu Palestina, uvamizi wa miaka 22 katika eneo la kusini mwa Lebanon na mzingiro wa mwaka saba sasa dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza, mbali na Wapalestina zaidi ya elfu tano wanaoshikiliwa kidhulma kwenye magereza ya Israel, yote hayo ni ushahidi tosha wa kudhihirisha dhati ya kivamizi ya utawala huo ghasibu unaojinasibu kuwa ni nchi ya kidemokrasia inayoishi na majirani zake pamoja na wafuasi wa dini za mbinguni kwa amani na masikilizano. Mnamo mwaka 1948, Wazayuni walijitengezea maskani katika ardhi iliyokuwa na watu wake na historia yake kongwe; na kwa kuwaua kinyama Wapalestina, kuwahamisha kwa nguvu katika majumba yao na kuwafanya wakimbizi, ndipo wakaweza kupora na kuikalia kwa mabavu miji na vijiji vya ardhi hiyo. Matokeo ya miongo sita ya kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu Palestina ni kutapakaa mamilioni ya wakimbizi wa Kipalestina katika kila pembe ya dunia pamoja na umwagaji damu uliotokana na vita kadhaa angamizi vilivyoanzishwa na Israel na kuliletea chungu ya maafa eneo hili la Mashariki ya Kati. Kutokana na makubaliano ya kimataifa pamoja na mikataba minne ya Geneva,  jamii ya kimataifa imetangaza mara kadhaa kuwa vitendo vinavyofanywa na askari wa Israel katika ardhi unazozikalia kwa mabavu si vya kibinadamu na ni sawa kabisa na jinai za kivita. Kupitishwa mamia ya maazimio katika Baraza la Usalama na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na taasisi za haki za binadamu na za utamaduni za umoja huo dhidi ya Israel yote hayo yanadhihirisha na kuthibitisha kwamba mfumo wa kimataifa unapinga na haukubaliani na  mwenendo unaokinzana na haki za binadamu wa utawala huo haramu…/

No comments:

Post a Comment