Wednesday, May 28, 2014

Uchaguzi wa Malawi wageuka 'Sarakasi

'

Shughuli ya kuhesabu kura ilirejelewa katika baadhi ya maeneo ya nchi Jumatatu kutoka na makosa mengi
Uchaguzi mkuu wa Malawi umeendelea kubeba sura mpya ya sarakasi za mapingamizi ya kisheria, baada ya mahakama kuu ya Lilongwe kuamuru Tume ya uchaguzi nchini humo iendelee na mipango ya kazi zake bila kuingiliwa na mamlaka yeyote.
Uamuzi huo umetokana na ombi la chama cha Malawi Congress MCP kutaka mahakama hiyo izuwie amri ya Mahakama kuu ya Blantyre iliyo iamuru tume ya uchaguzi kuhesabu kura na kumtangaza mshindi ndani ya siku 8, likiwa ni ombi la chama cha DPP.
Mwandishi wa BBC Baruan Muhuza aliye mjini Lilongwe anasema kuwa uamuzi huo sasa una maana kwamba MCP imeshinda kesi ambapo pamoja na mambo mengine wanataka kazi ya kuhesabu kura ianze upya nchi nzima jambo ambalo ndiyo maamuzi ya tume na vyama vyote vya siasa isipokuwa DPP.
Tume ya uchaguzi inakutana mjini Blantyre na itatoa taarifa baadaye kuhusu uamuzi uliochukuliwa na Mahakama Kuu hii leo.
Huku ikijulikana wazi kuwa kinachosubiriwa sasa ni ama kurudiwa kuhesabu kura za maeneo yenye mgogoro au kura zote za nchi nzima.
'DPP waja juu'
Rais Joyce Banda awali alitaka matokeo ya uchaguzi huo kufutiliwa mbali
Jumamosi mchana tume ya uchaguzi kwa pamoja na vyama vya siasa walikubaliana kurudia kuhesabu kura zote kutokana na kugundulika makosa mengi katika baadhi ya maeneo, huku DPP ikigomea hatua hiyo na kuamua kwenda mahakama kuu mjini Blantyre kuzuia mpango huo ikitaka zihesabiwe zile tu zinazotiliwa mashaka.
Jaji Lloyd Muhara wa mahakama hiyo alikubaliana na ombi la DPP jambo ambalo pia likazua upya mgogoro wa kisheria ambapo vyama vingine vikaungana kwa pamoja na wagombea binafsi kupeleka zuio kwenye mahakama kuu ya Lilongwe chini ya kundi la wanasheria zaidi ya 12 wa chama cha MCP.
'Wizi wa kura'
Vijana kwa wakongwe wote walijitokeza kushiriki uchaguzi huo ambao wadadis wanasema umegeuka sarakasi
Uchaguzi wa Malawi umekumbwa na wimbi la mivutano miongoni mwa vyama vikuu vya siasa vilivyo simamisha wagombea urais wa nchi hiyo.
Dalili za kujitokeza kwa matatizo zilianza mapema siku mbili baada ya uchaguzi ambapo baadhi ya vyama kikiwemo chama tawala Peoples Party cha Rais Dr Joyce Banda walilalamika kuwa kuna mchezo mchafu umefanyika katika shughuli nzima ya upigaji kura.
Siku chache zilizopita Rais Banda alitoa amari ya kuufuta uchaguzi huo na kuitisha uchaguzi mwingine baada ya siku 90 kwa madai ya wizi na ulaghai uliokumba uchaguzi, lakini Mahakama kuu ilisema hana mamlaka hayo.
Siku mbili baadaye tume ya uchaguzi MEC chini ya mwenyekiti wake Jaji Mackson Mbendera, ikatangaza kuwa ni kweli imegundua ubadhirifu katika baadhi ya maeneo na hivyo lazima kura zote zihesabiwe upya.
Kufikia sasa haijajulikana nini itakuwa hatma ya kura zilizopigwa na wananchi zaidi milioni saba wa nchi hiyo huku vyama vya DPP na MCP kila kimoja kikidai kuwa kilielekea kushinda uchaguzi huo.

No comments:

Post a Comment