Marekani hivi karibuni imewapa wapinzani wa serikali ya Syria aina mpya ya makombora ya kutungulia ndege yanayoweza kubebwa begani. Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon imetangaza kuwa hivi karibuni iliwapa wapinzani hao makombora mapya aina ya FIM-92 Stinger. Makombora hayo yana uwezo wa kulenga shabaha au chombo chochote kinachopaa kilichoko umbali wa mzunguko wa mita 4800 na urefu wa mita 180 hadi 3800. Kabla ya hapo Marekani ilikuwa tayari imekwishawapa wapinzani hao makombora ya kulenga vifaru na zana nyinginezo za kivita. Hii ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo kutangaza rasmi kwamba imewapa wapinzani wa Syria makombora aina ya stinger. Inaonekana kuwa lengo la Marekani kuwapa wapinzani silaha hizo ni kuimarisha uwezo wao wa kutungua ndege za kivita za serikali ya Damascus na hivyo kupunguza uwezo wa jeshi la Syria kuwashambulia kutokea angani.
Inaonekana kuwa baada ya kushindwa mazungumzo ya Geneva-2, nchi za Magharibi na hasa Marekani na Uingereza zimeamua kufuatilia njama zao za huko nyuma dhidi ya serikali ya Damascus, yaani ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya serikali na wakati huohuo kuwaimarisha kijeshi na kifedha wapinzani wa serikali ya Rais Bashar al-Asad wa Syria. Jambo hilo limekuwa likifuatiliwa na nchi hizo za Magharibi hasa baada ya kushika kasi harakati za kuandaliwa uchaguzi wa rais wa Syria mwaka huu. Mara tu baada ya kuanza vita vya ndani vya Syria, Marekani na waitifaki wake wa Magharibi pamoja na nchi za Kiarabu, zilianzisha njama kubwa za kuingusha serikali ya Damascus, kwa kutoa misaa mikubwa ya kifedha, silaha, habari za kijasusi na mafunzo ya kijeshi kwa wapinzani. Hii ni katika hali ambayo ushindi wa kijeshi na wanamgambo wa Syria katika maeneo tofauti ya nchi hiyo kwa upande mmoja na kuongezeka vitendo vya ukatili vya makundi ya kitakfiri nchini humo kwa upande wa pili kumeondoa kabisa uwezekano wa kupatikana ushindi wa kijeshi katika vita vya ndani vya Syria. Lakini Marekani na waitifaki wake wa Kimagharibi wamefumbia macho ukweli huo na kurejelea siasa zao zilizofeli za kutoka mashinikizo ya kijeshi dhidi ya serikali halali ya Damascus. Kuhusiana na suala hilo katikati ya mwezi Februari mwaka huu, Rais Barrack Obama wa Marekani alifichua siasa za kichochezi za Washington dhidi ya serikali halali ya Syria kwa kusisitiza kuwa, mashinikizo makubwa na ya haraka yanapaswa kutolewa dhidi ya serikali ya Rais Bashar al-Asad kwa kushirikiana na kila kundi linaloipinga serikali yake. Kwa hakika lengo la Wamagharibi ni kuyaimarisha makundi ya kigaidi yanayopigana na serikali ya Syria ili kwa njia hiyo yaweze kuvuruga mkondo mzima wa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo na wakati huohuo kuandaa uwanja wa kubanwa serikali ya Damascus na kuifanya ilegeze msimamo na kutoa fursa kubwa kwa wapinzani katika mazungumzo ya baadaye. Pamoja na hayo yote lakini serikali ya Syria imethibitisha kivitendo kuwa haiko tayari kupiga magoti mbele ya mashinikizo ya Wamagharibi na washirika wao wa Kiarabu na imeazimia kupambana vilivyo na makundi ya kigaidi ili kurejesha amani na utulivu wa kudumu nchini humo.
No comments:
Post a Comment