Olusegun Obasanjo Rais wa zamani wa Nigeria ameanza juhudi za kufanya mazungumzo na shakhsia walio karibu na kundi la Boko Haram kwa lengo la kuwakomboa wanafunzi wasichana wanaoshikiliwa mateka na kundi hilo kwa zaidi ya siku arubaini sasa. Vyombo vya habari vimetangaza leo kuwa, Obasanjo ameanzisha juhudi hizo ili kuzuia kufanyika operesheni za kijeshi ambazo huenda zikahatarisha maisha ya wanafunzi hao. Rais mstaafu wa Nigeria ameingiwa na wasiwasi na uamuzi wa serikali ya Abuja wa kuomba msaada kutoka madola ya kigeni katika operesheni ya kutaka kuwaokoa wanafunzi hao waliokamatwa mateka tokea mwezi uliopita. Wakati huohuo, duru za habari kutoka Nigeria zimeripoti kuwa, mmoja kati ya wanafunzi hao waliokamatwa mateka amefanikiwa kutoroka mikononi mwa wanamgambo wa Boko Haram na kusema kwamba, kati ya wanafunzi 280 wa shule ya Chibok waliokamatwa mateka, 50 kati yao walifanikiwa kutoroka. Hivi karibuni, Dakta Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran alilaani misimamo ya kundi lenye misimamo mikali la Boko Haram na kusisitiza kwamba, lengo la kundi hilo ni kuchafua taswira nzuri ya dini tukufu ya Kiislamu na kuyapatia mwanya madola ya kigeni kuingilia masuala ya ndani ya Nigeria.
No comments:
Post a Comment