Wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, wamewaua Waislamu 11 mjini Bangui na miji mingine ya nchi hiyo ndani ya kipindi cha siku tatu. Kwa mujibu wa ripoti ya Kamisheni ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa UNHCR , mwezi uliopita jumla ya watoto wa Kiislamu 29 wakiwa na wazazi wao ambao walikuwa wamekimbilia nchini Cameroon ili kuokoa maisha yao kutokana na mauaji ya kikabila nchini mwao, walipoteza maisha kutokana na kukosa chakula, maji, mchoko na joto kali. Karibu Waislamu laki moja na elfu 10 wa Jamhuri ya Afrika ya Kati walielekea nchini Cameroon baada ya kushadidi mauaji ya magaidi wa Anti-Balaka dhidi yao miezi minne iliyopita. Hii ni katika hali ambayo msemaji wa jumuiya ya Waislamu wa nchi hiyo, ametangaza kuwa, jinai na mauaji ya wanamgambo hao wa Kikristo yanafanyika kwa uungaji mkono wa Ufaransa, huku akikosoa hatua ya jamii ya kimataifa ya kufumbia macho jinai hizo zinazotendeka bila ya uficho. Zaidi ya watu 2000 wameuawa katika vitendo vya ukatili na jinai tofauti huku wengine wapatao milioni moja kati ya jamii nzima ya watu milioni nne na laki tano wanaounda jamii ya nchi hiyo wakiwa wamelazimika kuyakimbia makazi yao licha ya kuwepo vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na askari wa Ufaransa.
No comments:
Post a Comment