UCHAGUZI
wa Simba umepamba moto, kila mdau ndani ya klabu hiyo lakini hata wadau wengine
kwenye mchezo wa soka nchini wana hamu ya kutaka kujua kuwa nani atakuwa rais wa
kwanza wa Simba.
Kwa
mara ya kwanza kiongozi wa juu atakayepatikana atatumia cheo cha rais tofauti na
hapo awali alikuwa akitumia kile cha mwenyekiti na msaidizi wake makamu
mwenyekiti wakati wa sasa atajulikana kama makamu wa
rais.
Bado
suala la majina ya vyeo linaweza lisiwe kubwa sana kwa wanachama hao, lakini
wanachotaka kuona ni kiongozi bora ambaye ataiongoza timu hiyo kutoka kwenye
kipindi kigumu cha kuwa timu mambo yake yaliyokwenda
shaghalabaghala.
Kila
mmoja anajua, sasa si siri tena kwamba wakati wa Ismail Aden Rage, Simba
imeporomoka kwa kiasi kikubwa licha ya kwamba klabu iliingiza fedha nyingi
kupitia kwa wadhamini na hata mapato mazuri.
Kipindi
ambacho Simba ilifeli kimipango, uongozi haukuwa na ubunifu, haukuwa na umakini
ndiyo maana hadi leo fedha za mauzo ya Emmanuel Okwi dola 300,000 (Sh milioni
480), Simba hawajaambulia hata senti zaidi ya stori na ahadi za mwenyekiti wao
anayemaliza muda wake.
Hakuna
Mwanasimba atataka yatokee tena yale ya katika kipindi cha Rage, maana ndiyo
wakati mgumu zaidi katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi. Kipindi cha
manyanyaso na mambo kwenda kwa kubahatisha.
Lakini
wakati mchakato wa uchaguzi ukianza kuchukua hatua, Rage amekuwa akijitokeza na
kuonyesha wazi anapiga debe, ameonyesha anamtetea mgombea mmoja, kitu ambacho si
kizuri pia ni dalili za kuingilia kazi za kamati ya uchaguzi ambayo inapaswa
kuwa huru.
Nilisikia
baadhi ya wanachama wamekuwa wakisema hivi, hakuna sababu ya kuenguliwa kwa
mgombea na badala yake kamati iache kila mtu akapambane kwa kura. Hilo ni wazo
zuri, lakini wanaosema niliona hawakutafakari kwa kuwa sheria zinafuata
mkondo.
Kamati
haina uwezo wa kumkatia mtu rufaa, badala yake inazishughulikia rufaa
zilizokatwa na wanachama. Vema wawashauri wale wanaotaka kukata rufaa wasifanye
hivyo na si kuiambia kamati iache kufanya hivyo!
Lakini
ajabu, Rage naye amekaririwa na gazeti la Tanzania Daima la jana akimtetea
mgombea wa Urais Simba, Michael Wambura kwamba hakuwahi kufukuzwa Simba au hata
tatizo lolote. Hiyo si kazi yake sasa, aiachie
kamati.
Kamati
ya uchaguzi ya Simba inaongozwa na Dokta Damas Daniel Ndumbaro ambaye ni mmoja
wanasheria mahiri, maarufu nchini. Ni mwalimu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM)
ambako anafundisha sheria, pia mwalimu katika Chuo Kikuu Huria cha Dar es
Salaam, pia aliwahi kuwa wakala wa kuuza wachezaji anayetambuliwa na
Fifa.
Sasa
vipi Ndumbaro ashindwe kuwa makini na maneno, maana yangu kitu ambacho si sahihi
au sahihi kuhusiana na tuhuma kuhusu Wambura au mgombea yeyote aliyekatiwa rufaa
atashindwa kung’amua vipi? Bado kamati hiyo ina wanasheria na watu wengine
makini. Tatizo la Rage kuanza kuzungumzia mambo ambayo kama yakitokea
yataamuliwa na kamati ni lipi?
Rage
anyamaze, aache kamati ifanye kazi yake kwa uhuru bila ya kubugudhiwa kwa kuwa
ina wanasheria wa kutosha ambao wanajua kipi cha kufanya. Hakuna anayeweza
kumuonea Wambura kwa kuwa kila kitu kiko wazi, ikitokea kaonewa, watu wataona na
kuna vyombo vinaweza kulitatua hilo kwa mujibu wa kanuni na sheria lakini
mwenyekiti kuwahi na mapema kuonekana ukitetea au kutaka kuifumba kamati
mdomo!
Kamati
iachwe iwe huru, ili ifanye kazi yake bila ya mashinikizo. Lakini pendekezo kwa
mwenyekiti wa kamati na wajumbe wake, lazima wachukue uamuzi ambao hautakuwa
unammyima haki mtu yoyote. Wanachoona sahihi ndiyo wapiti hicho bila ya kujali
Rage alizungumza hivi, au fulani anafanya vile. Haki ndiyo itaisaidia Simba,
kuonea au kukandamazi, kutasababisha Simba iendelee kukandamizwa kama ilivyokuwa
miaka minne iliyopita.
No comments:
Post a Comment