Nchini Misri ripoti zinasema kuwa ni watu wachache sana waliojitokeza katika siku ya pili na ya mwisho ya kupiga kura katika uchaguzi wa rais huku mkuu wa zamani wa jeshi Abdul Fattah el-Sisi akitazamiwa kuibuka mshindi katika uchaguzi huo.
Serikali ya Misri imetangaza leo Jumanne kuwa siku ya mapumziko kitaifa ili kujaribu kuwashawishi watu wajitokeza kupiga kura lakini pamoja na hayo idadi ya wapiga kura imekuwa ndogo sana. Uchaguzi huo wa rais una wagombea wawili tu yaani el-Sisi na mwanasiasa wa mrengo wa kushoto Hamdeen Sabahi.
Wafuasi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin awali walitangaza kususia uchaguzi huo wa rais wakisema uchaguzi huo hauwezi kuhalalisha uhalifu. Wamesema hayo katika kumuashiria Abdul Fattah el-Sisi ambaye alikuwa mkuu wa jeshi wakati rais wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasia Mohammad Morsi alipoondolewa madarakani mwezi Julai mwaka jana. Kwingineko Msemaji wa Ikhwanul Muslimin amesema kuwa, el Sisi ni kopi ya Hosni Mubarak dikteta aliyeondolewa madarakani nchini humo. Abdul-Mawjood Dardiri ameongeza kuwa uchaguzi wa Misri ni kiini macho na kusisitiza kwamba, demokrasia imetoweka baada ya wanajeshi kudhibiti vyombo vyote vya dola.
No comments:
Post a Comment