RIVALDO
alifanikiwa kushinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ulaya, mara tu baada ya mafanikio
hayo akaamua kuanika hisia zake na kumwambia kocha wake kwamba hatacheza tena
upande wa kushoto, yaani winga. Badala yake anataka kucheza namba
kumi.
Kocha
wake katika kikosi cha Barcelona wakati huo akamuambia sawa, wakati unachukua
tuzo ya mchezaji bora ulikuwa unacheza kama winga wa kushoto, sasa umevimba
kichwa, utakula jeuri yako. Rivaldo akaanza kusota benchi, hadi aliposalimu amri
na kukubali kucheza winga ya kushoto.
Kocha
huyo alikuwa ni Luis van Gaal, bosi mpya wa Manchester United ambaye anaaminika
anafanana na Alex Ferguson kiutendaji na hasa namna ya kufanya kazi na mastaa
wakubwa.
Van
Gaal aliyekuwa Kocha Bora wa Dunia mwaka 1995 si mtu wa kubabaika, anaijua kazi
yake, pia ni mwenye msimamo wa anachotaka, lakini anavutiwa kuwa na urafiki na
wachezaji wake.
Kikubwa
ambacho wengi wanataka kujua ni kuhusu nini atakifanya kuibadilisha Manchester
United ambayo ni mfupa uliomshinda David Moyes baada ya Ferguson ‘kuula’ kwa
raha zake, tena kwa ulaiini.
Kushindwa
hakitakuwa kitu rahisi kwa maana ya rekodi, maana van Gaal ameshinda karibu
mataji yote, ukianza na ubingwa wa Uholanzi akiwa na Ajax, ule wa La Liga akiwa
na Barcelona, pia bingwa wa Bundesliga akiwa na Bayern
Munich.
Usisahau
Kombe la Washindi Ulaya na Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo hana ugeni hata kidogo
na makombe, ingawa si ‘garantii’ kwamba kupitia rekodi zake leo ndiyo atashinda
tena.
Kinachowaumiza
kichwa wengi ni mfumo, kawaida van Gaal ‘anaabudu’ ule wa 4-3-3 ambao utakuwa ni
mpya na mgumu kwa wachezaji wa Manchester United.
Hata
sasa akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya Uholanzi, van Gaal amekuwa akiutumia
zaidi mfumo huo kama namna moja kwake, lakini ana tabia nyingine ya kujaribu
mifumo.
Kawaida
van Gaal anasema anataka kutumia mfumo kutokana na wachezaji. Kwa Manchester
United, 4-4-2 umekuwa ndiyo mfumo mama, lakini kwake ni nadra, huenda akaujaribu
pia.
Lakini
amekuwa akitumia mifumo mingine na kuwashangaza wengi, mfano wakati akiwa na
Barcelona, amewahi kutumia mfumo wa 2-3-2-3.
Manchester
United wataweza mfumo huo?
Atawatumia
akina nani na ukizingatia safu ya ulinzi imeporomoka na kwa mfumo wake lazima
awe na wachezaji wakongwe?
Hana
namba sita wa uhakika, Michael Carrick ataingia kwenye mfumo wake? Akiwa
Barcelona aliwatumia zaidi wachezaji wake wakati huo Pep Guardiola na Puyol
kwenye ukabaji, anahitaji wachezaji wa namna hiyo.
Ili
kuingiza mifumo anayotaka, van Gaal analazimika kufanya usajili hasa kwenye
kiungo ambako Kroos kutoka Bayern anamfaa, lakini beki mkongwe angalau mmoja wa
kusaidiana na Chris Smalling, John Evans na Phil
Jones.
No comments:
Post a Comment