Tuesday, May 27, 2014

Umoja ni hitajio la dharura la ulimwengu wa Kiislamu'

  • Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei
    Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema, umoja na kuundwa umma ulio shikamana ni hitajio la dharura katika Ulimwengu wa Kiislamu. Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo Jumanne mjini Tehran kwa mnasaba wa Idi ya Mabaath (Kupewa utume Mtume Muhammad SAW) wakati alipokutana na wakuu wa mfumo wa Kiislamu, wananchi wa matabaka mbali mbali, washiriki wa Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani na mabalozi wa nchi za Kiislamu. Katika kikao hicho, Kiongozi Muadhamu alisisitiza kuwa, moja kati ya malengo asili ya wanaoibua hitilafu miongoni mwa Waislamu na kuchochea chiku dhidi ya Ushia na Iran ni kuficha matatizo ya kambi ya madola yenye kiburi na kuulinda utawala ghasibu wa Kizayuni. Amesema ili kutambua vizuri hali halisi ya mambo, mataifa ya Waislamu na hasa wasomi na wanazuoni wa umma wa Kiislamu wanapaswa kuwa na tadbiri, uono wa mbali na kutambua kwa njia sahihi kambi ya maadui wa umma wa Kiislamu. Ayatullah Khamenei amesema hitajio jingine muhimu la ulimwengu wa Kiislamu ni kutafakari, kuwa na busara na kutambua ipasavyo kambi ya maadui wa ummah wa Kiislamu sambamba na kuungana na pia kujiepusha na hitilafu za kiitikadi na kikaumu. Amesisitiza kuwa, leo bendera azizi ya Uislamu inapepea huku zikiimarika hisia za utambulisho wa Kiislamu miongoni mwa Waislamu duniani. Kwingineko katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu ameonya kuhusu ufahamu potofu na wa kijuu juu wa Uislamu na aya za Qur'ani. Aidha ameashiria kuhusu njama za maadui wanaokusudia kuharibu sura halisi ya Uislamu. Ayatullah Khamenei ametoa mfano wa yanayojiri barani Afrika na kusema, leo kuna sehemu ambayo Waislamu wanadhulumiwa na kuuawa kwa umati na katika nchi nyingine ya Kiafrika kuna wale ambao kwa jina la Uislamu wamewachukua wasichana mateka. Ameongeza kuwa leo adui amejitokeza wazi wazi katika vita vyake dhidi ya Uislamu na chombo muhimu zaidi wanachotumia na kuibua hitilafu za kiitikadi na vita baina ya Shia na Sunni. Ayatullah Khamenei amesema iwapo busara zitatumika basi Waislamu wanaweza kumzuia adui kufikia malengo yake. Kiongozi Muadhamu amesema nchi za Magharibi zinahimiza ujahili ambao Mtume Muhammad SAW alibaathiwa kuuangamiza. Amesema ukosefu wa uadilifu, ubaguzi, kupuuzwa heshima ya mwanaadamu, na kuwahimiza wanawake kuelekea katika ufasiki yote hayo ni dhihirisho la ustaarabu wa kifisadi na kwa hakika ni kurejea katika ujahilia lakini kwa kutumia mbinu za kisasa. Kiongozi Muadhamu pia ameashiria njama za kukandamizwa mwamko wa Kiislamu na kusema mwamko wa Kiislamu hauwezi kukandamizwa. Ayatullah Khamenei amesema siri ya ushindi wa Mfumo wa Kiislamu Iran katika nyuga za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimataifa ni kuamini na kuwa na dhana nzuri kuhusu ahadi ya Mwenyezi Mungu. Amesema hiyo ndio njia ya taifa la Iran na itaendelea kuwa vivyo hivyo.

    No comments:

    Post a Comment