Taasisi ya Pride Tanzania ambayo ilianzishwa kwa lengo la kutoa mikopo midogo midogo kwa wajasiriamali imetoweka kwenye orodha ya mali zinazomilikiwa na Serikali.
Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inasema taasisi hiyo ilianzishwa Mei 5 mwaka 1993 chini ya Sheria ya Makampuni (CAP 212) kwa dhamana.
Dhumuni la kuanzisha taasisi hiyo ni kutoa mikopo midogo midogo kwa wajasiriamali.
“Chanzo kikuu cha fedha za kuanzisha taasisi hii kilitoka shirika la Maendeleo la Norway (NORAD) kwa makubaliano baina ya Serikali za Tanzania na Norway,” inasema taarifa hiyo.
CAG anasema taarifa za Msajili wa Hazina inaonyesha kuwa uwekezaji wa Serikali katika kampuni kufikia Juni 30 mwaka 2008, hisa zote za Pride zinamilikiwa na Serikali.
Taarifa hiyo inasema mtaji hadi Juni 30 mwaka 2008, unaonyesha kuwa ni Sh2.301 bilioni na fedha za wanahisa wengine zilikuwa ni jumla ya Sh2.198 bilioni na hivyo kuufanya mtaji mzima kuwa Sh4.499 bilioni.
“Kwa mujibu wa taarifa ya msajili wa hazina iliyoishia Juni 30 mwaka jana, shirika hili halipo tena kwenye orodha ya mashirika ya umma,” anasema.
Hata hivyo, anasema uhalali na sababu za kuondolewa kwa shirika hilo katika orodha ya msajili wa kampuni hazikufahamika.
CAG anasema aliandika barua yenye kumbukumbu namba CB.27/31/63 Juni 20 mwaka juzi ili kupata maelezo juu ya umiliki wa Pride Tanzania, lakini hadi sasa haijajibiwa.
Kwa mujibu wa kifungu cha 31 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma namba 11 ya mwaka 2008, kila shirika la umma linatakiwa kupeleka hesabu kwa CAG kukaguliwa katika kipindi cha miezi mitatu baada ya mwaka wa fedha kukamilika.
Hata hivyo, hesabu za Pride Tanzania hazijawahi kuwasilishwa kwa CAG kama inavyotakiwa kisheria, jambo linaloibua maswali kwa Watanzania.
No comments:
Post a Comment